Wednesday, August 11, 2010

BONGO.......!

Jamani narudi tena katika ulingo huu wa wanaopenda kusemasema, maana hata mtembea bure si sawa na mkaa bure......japo siku moja nilikuwa juu ya mawe.."bankrupt" nikakumbuka usemi huu nikatoka nyumbani kwenda kutembea nikiwa na tumaini la kupata chochote, sikuona huo muujiza. Rafiki yangu kuna misemo mingine ya kiswahili inaweza kukuingiza chaka.

Naomba uchanganuzi wa maneno haya ambayo yanatumiwa sana na watanzania wengi.
  • mtu akisema BONGO anamaana sawa na jina la nchi, yaani TANZANIA?
  • nini wingi wa neno UBONGO?
  • Je! kuna uhusiano wowote wa kilugha kati ya neno BONGO na UBONGO? eleza kidogo.
  • wengi husema ukiishi bongo lazima uchangamshe ubongo maana bongo ni kwa wajanja tu....! kuna uhusiano wowote wa usemi huu na hali halisi ya watanzania waishio bongo?
 Karibu kwenye shamba darasa lisilojali umri wa mtahiniwa.......elimu ni bahari.

ELIMU YETU.


Ni takribani miaka 40 sasa tangu tupate uhuru Tanzania. Sekta ya elimu imepiga hatua nyingi ikiwemo kaulimbiu ya ujenzi wa shule za kata. Changamoto nazo zimepiga hatua sambamba na wingi wa shule.
Inasikitisha kuona bado idadi kadhaa ya wanafunzi wa shule za sekondari wanakaa chini wakati wa kufundishwa na hata wakati wa mitihani yao. Kwa hali hii ufaulu wa wanafunzi utaongezeka? kwa nini wanafunzi wakifeli jamii inamtazama mwalimu kama chanzo cha tatizo? Ikumbukwe kwamba kuna mambo mengi yanayoweza kuchangia mwanafunzi kufaulu, sio juhudi ya mwalimu pekeyake.
Nchi yetu inautajiri wa kutosha kama madini, mbuga za wanyama, uvuvi, kilimo, misitu nk. Hazina hii inatosha kuboresha uchumi bila kusahau sekta ya elimu. Tuna wasomi wengi na watalamu ndani na nje ya nchi, wakipewa nafasi katika uboreshaji wa elimu tutapiga hatua zaidi.
Sasa ni wakati wa kampeni za uchaguzi wa madiwani, wabunge na uraisi. Je! wagombea watatoa sera gani katika kuinua kiwango cha elimu? Tafiti nyingi za elimu zimefanywa zikiwa na mapendekezo mengi juu ya njia mbadala za kuboresha elimu yetu, matokeo yake tafiti hizi zinarundikana kwenye kabati za taasisi mbalimbali kikiwepo chuo kikuu cha Dar es salaam. Tafiti zimekuwa zikifanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ili kutimiza masharti ya kupa degree, master na PhD……baada ya hapo ‘research reports’ hizi hufungiwa kwenye masanduku.
Hatuwezi kunyoshea kidole mtu Fulani au kikundi cha watu, bali Watanzania wote tuamke na kupiga vita hali duni ya elimu katika nchi yetu. 
Shule hizi za kata zitakuwa na mafanikio kama watoto wote wa viongozi wakuu selikarini  watapeleka watoto wao huko wakachanganyike na watoto wetu kwenye shule zisizo na maabara na uhaba wa walimu.