Hatimaye chama cha walimu Tanzania ( CWT ) kimethibitisha kuwa mgomo wa walimu nchi nzima uko palepale kuanzia jumatatu tarehe 31-julai-2012. Rais wa CWT, Gratian Mukoba ameitaka serikali kuacha vitisho dhidi ya walimu. Aidha mgomo huo utakuwa halali baada ya serikali kupewa notisi ya saa 48 iliyoanza saa 8 mchana ijumaa na kuisha saa 8 mchana jumapili kisha kutangaza rasmi mgomo huo kuanzia jumatatu.
Madai ya walimu ni pamoja na ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia kwa walimu wa sayansi asilimia 55, asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya sanaa na posho kwa walimu wanaoishi katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa chapisho la gazeti la Mwananchi la tarehe 29-7-2012, kauli ya Wizara kupitia kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo alipoulizwa kuhusu uamuzi wa walimu kuendelea na mgomo,
alisema hawezi kuzungumzia hilo yuko safarini kuelekea Mbeya.
“Siwezi kuzungumza nipo safarini kuelekea Mbeya na hatuwezi kuelewana hivyo, mtafute Waziri atazungumzia,” alisema Mulugo.
Hata
hivyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa
alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokewa.
Kutokana na gharama za maisha kuwa ngumu kw watanzania wa kipato cha chini, ni dhahiri kuwa kuna umuhimu kwa walimu kusikirizwa madai yao. Hata waheshimiwa wabunge walikiri kuwa hali ya maisha ni ngumu, lakini walighubikwa na ubinafsi pali waliposema kuwa gharama za maisha mjini Dodoma ni kubwa hivyo wao waongezewe posho. Kama Dodoma maisha ni magumu, je! watanzania wengine waishio hapo Dodoma na mikoa mingine wao nani atawanusuru na hii hali ya maisha magumu? Tunaomba Serikali itambue kuwa hata watumishi wengine wa uma kama walimu, polisi, wauguzi, n. k. wanahitaji kuboreshewa mishahara yao ili kukabiliana na mfumuko wa gharama za maisha.