Wednesday, September 15, 2010

Life after college

Mara nyingi maisha baada ya chuo huwa magumu kwa baadhi ya wahitimu. Hili tatizo huja pale mhitimu anapokuwa amejipangia malengo yake ya kimaisha lakini mwajiri wake hugeuka kuwa mbogo mahali pa kazi.

Kumekuwa na manyanyaso mengi katika vituo vingi kwa watumishi pale wakuu wa vituo wanapowabana wahitimu wengi kukosa nafasi za kuhudhuria semina mbalimbali za watumishi, kuishi ndani ya kituo bila kupata nafasi ya kwenda nje ya kituo. Wasiwasi wa wakuu wengi kuogopa kuporwa madaraka yao na watumishi katika vituo vyao waliojiendeleza limekuwa tatizo mojawapo linalofanya waishi kwa shida.
Wahitimu wengi kutoka vyuo vikuu hujikuta hawatimizi malengo yao na mazingira ya kazi kuzidi kuwa magumu kwao. Swali linabaki kwa hawa wakuu wa vituo vya taasisi mbalimbali kuwa kwa nini wasitumie muda wao kujiendeleza kielimu badala ya kuendelea kugombana na watumishi?

Wednesday, August 11, 2010

BONGO.......!

Jamani narudi tena katika ulingo huu wa wanaopenda kusemasema, maana hata mtembea bure si sawa na mkaa bure......japo siku moja nilikuwa juu ya mawe.."bankrupt" nikakumbuka usemi huu nikatoka nyumbani kwenda kutembea nikiwa na tumaini la kupata chochote, sikuona huo muujiza. Rafiki yangu kuna misemo mingine ya kiswahili inaweza kukuingiza chaka.

Naomba uchanganuzi wa maneno haya ambayo yanatumiwa sana na watanzania wengi.
  • mtu akisema BONGO anamaana sawa na jina la nchi, yaani TANZANIA?
  • nini wingi wa neno UBONGO?
  • Je! kuna uhusiano wowote wa kilugha kati ya neno BONGO na UBONGO? eleza kidogo.
  • wengi husema ukiishi bongo lazima uchangamshe ubongo maana bongo ni kwa wajanja tu....! kuna uhusiano wowote wa usemi huu na hali halisi ya watanzania waishio bongo?
 Karibu kwenye shamba darasa lisilojali umri wa mtahiniwa.......elimu ni bahari.

ELIMU YETU.


Ni takribani miaka 40 sasa tangu tupate uhuru Tanzania. Sekta ya elimu imepiga hatua nyingi ikiwemo kaulimbiu ya ujenzi wa shule za kata. Changamoto nazo zimepiga hatua sambamba na wingi wa shule.
Inasikitisha kuona bado idadi kadhaa ya wanafunzi wa shule za sekondari wanakaa chini wakati wa kufundishwa na hata wakati wa mitihani yao. Kwa hali hii ufaulu wa wanafunzi utaongezeka? kwa nini wanafunzi wakifeli jamii inamtazama mwalimu kama chanzo cha tatizo? Ikumbukwe kwamba kuna mambo mengi yanayoweza kuchangia mwanafunzi kufaulu, sio juhudi ya mwalimu pekeyake.
Nchi yetu inautajiri wa kutosha kama madini, mbuga za wanyama, uvuvi, kilimo, misitu nk. Hazina hii inatosha kuboresha uchumi bila kusahau sekta ya elimu. Tuna wasomi wengi na watalamu ndani na nje ya nchi, wakipewa nafasi katika uboreshaji wa elimu tutapiga hatua zaidi.
Sasa ni wakati wa kampeni za uchaguzi wa madiwani, wabunge na uraisi. Je! wagombea watatoa sera gani katika kuinua kiwango cha elimu? Tafiti nyingi za elimu zimefanywa zikiwa na mapendekezo mengi juu ya njia mbadala za kuboresha elimu yetu, matokeo yake tafiti hizi zinarundikana kwenye kabati za taasisi mbalimbali kikiwepo chuo kikuu cha Dar es salaam. Tafiti zimekuwa zikifanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ili kutimiza masharti ya kupa degree, master na PhD……baada ya hapo ‘research reports’ hizi hufungiwa kwenye masanduku.
Hatuwezi kunyoshea kidole mtu Fulani au kikundi cha watu, bali Watanzania wote tuamke na kupiga vita hali duni ya elimu katika nchi yetu. 
Shule hizi za kata zitakuwa na mafanikio kama watoto wote wa viongozi wakuu selikarini  watapeleka watoto wao huko wakachanganyike na watoto wetu kwenye shule zisizo na maabara na uhaba wa walimu.

Thursday, July 22, 2010

VUVUZELA IMEANZA ENZI ZIPI?



Historia inasemaje?


Kumekuwa na maswali mengi kuhusu asili au chanzo cha vuvuzela , chombo kilichotumika kama sehemu ya burudani hivi karibuni huko bondeni. Je! unajua chimbuko lake au hawa wanasingiziwa tu? kama itakuwa kweli unajifunza nini ?
Je! hii inakamilisha usemi usemao "USILOLIJUA NI KAMA USIKU WA GIZA"

Tuesday, July 13, 2010

Ngoma zetu.

Historia inaonesha babu na bibi zetu walikuwa na utamaduni asilia, lakini kizazi cha leo kimebebwa na mitindo ya utamaduni wa kigeni. Bila shaka maamuzi ya kizazi kipya kama miziki yao inavyojitambulisha yalikuwa sahihi kutokana na sabubu walizoziona wao.

Ukiangalia kipande hiki cha ngoma asilia ijulikanayo kama "acrobatic snake dance" utaona radha tofauti na ubora wa tamaduni za wahenga wetu. Ngoma au utamaduni wetu wa asili ulikuwa unatukumbusha mambo mengi ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiimani na hata kutuelimisha kisaikolojia. Utamaduni wa kigeni kutoka "ughaibuni" una radha tofauti na isiyokidhi hali halisia ya mazingira yetu tulolisishwa na babu zetu.


Utandawazi unatuweka sote kama kijiji kimoja lakini swali lakujiuliza ni kuangushwa kwa utamaduni wetu wa kiafrika na kujikuta tunakuwa na utandawazi ulojaa sura moja ya vionjo vya kiutamaduni.
Mimi nafikiri tuige mfano wa kaa (au crab) anayejongea kwa kwenda mbele na nyuma pia. Tusisahau tutokako japo kuna umhimu wa kutazama tuendako. Mtu huenda akawa si jasiri sana kama hajiamini au hawezi kujivunia hata kile kidogo alichonacho. MUNGU KATUJALIA MAMBO MENGI WAAFRIKA TUJIAMINI NA TUULINDE UTAMADUNI WETU.

Monday, July 12, 2010

Karibuni ndugu!

Nawakaribisha kwenye kibaraza hiki, nikiwa mgeni kidogo, natambua umuhimu wa kubadilishana mawazo kuelimisha na kuburudisha kuwa ndio msingi mkubwa wa IT. Kwa kiasi nategemea uwepo wenu mtandaoni uwe na msaada kwa wanaoanza na sio kuwa na mtazamo wa kujuana. Karibuni sana